SERIKALI YATENGA SHILINGI MILIONI 960 UJENZI WA MABWENI
DODOMA
SERIKALI imeelekeza fedha kiasi cha sh. milioni 960 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya sherehe za uhuru mwaka huu sasa zitumike kujengea mabweni katika shule nane za msingi za wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Akizungumza na wandishi habari jijini Dodoma Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge George Simbachawene amesema agizo hilo limetolewa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan huku akisisitiza kuwa sherehe za mwaka huu hakutokuwa na gwaride na shughuli nyingine za kitaifa.
Simbachawene amezitaja shule hizo kuwa ni shule ya msingi Buhangija (Shinyanga), Goweko (Tabora),Darajani (Singida), Mtanga (Lindi), Songambele (Manyara), Msanzi (Rukwa), Idofi (Njombe), na shule ya msingi Longido (Arusha).
"Naomba kutumia fursa hii kwa namna ya kipekee sana, kumshukuru na kumpongeza Rais Dk. Samia kwa kuelekeza fedha kiasi cha sh. milioni 960 zilizokuwa zimetengwa na wizara na taasisi kwa ajili ya maadhimisho ya sherehe za uhuru mwaka huu zipelekwe TAMISEMI na zitatumika kujenga mabweni katika shule nane za msingi za wanafunzi wenye mahitaji maalum,"alisema
Simbachawene amesema hiyo ni dhamira ya dhati ya Rais Samia kuwajali na kuwajengea mazingira rafiki watu wenye mahitaji maalum hapa nchini.
Pia amebainisha maadhimisho ya sherehe za miaka 61 ya uhuru wa Tanzania bara mwaka huu zitafanyika kwa midahalo na makongamano mbalimbali yatakayofanyika katika wilaya zote hapa nchini kujadili, kutafakari kwa pamoja .
Kwa mujibu wa Simbachawene amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza TAMISEMI kufanya usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya midahalo na makongamano hayo ili kujiridhisha na matokeo yake.
Comments
Post a Comment