WAHITIMU WA CHUO WAASWA KUJIFUNZA KWA WALIOFANIKIWA ILI WAFANIKIWE.
Pichani: Wahitimu wa chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kilichopo Jijini Dodoma wa Kozi mbalimbali waliohudhulia kwenye Mahafali ya 36.
Wahitimu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kilichopo Jijini Dodoma wameaswa kujikita katika malengo yao na kuacha kuangalia walioshindwa na kuanguka badala yake wajifunze kwa waliofanikiwa ili na wao waweze kuwa wenye mafanikio.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi Jenifa Omolo akiwa mgeni rasmi aliyemwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Mwigulu Lameck Nchemba katika mahafali ya 36 ya chuo hiki cha Mipango ya Maendeleo Vijijini yaliyofanyika Jijini Dodoma.
"Msiwe na mawazo tofauti kwamba kuna mwingine alihitimu mwaka jana na hajapata kazi, wewe jikite kwenye malengo yako usiangalie mtu kaanguka, kila mtu ana malengo yake. Mwingine alianza biashara kaanguka wewe hiyo sio kazi yako hujui kilichomfanya aanguke,watu wameanza makampuni wameshindwa kuendelea . Usiangalie kufeli angalia mafanikio hapo utafanikiwa,usiangalie jirani yako ameanzisha sijui kitu gani kimeanguka ,usiende kujifunza huko, jifunze kwa waliofanikiwa"
Aidha Bi Jenifa amewataka Wahitimu na wale wanafunzi watakaoendelea na mafunzo kwa ngazi ya juu kuwa na chachu ya kuendelea kujifunza ili kuongeza maarifa,ujuzi na ubunifu unaohitajika katika kuboresha utendaji wao wa kazi.
"Ni matumaini yangu kuwa mtathibitisha vema maarifa ya ujuzi mliyopa hapa Chuo cha Mipango Kwenye ulimwengu wa kazi, niwakumbushe kuwa mafanikio katika ulimwengu wa leo wa kazi yanahitaji moyo wa kupenda kuendelea kuwa na chachu ya kujifunza ili kuongeza Maarifa,Ujuzi na Ubunifu unaohitajika katika kuboresha utendaji wenu wa kazi"
"Na kuongeza kuwa, na wale mtakaoendelea na ngazi ya juu katika masomo Nawaasa mkaendelee kujifunza kwa bidii ili kupata maarifa na ujuzi utakaowezesha kuhimili Mazingira ya ulimwengu wa kisasa kwa kazi ya Maendeleo ya kiuchumi ya Familia zetu na Taifa kwa ujumla".
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Mipango Vijijini Prof. Hozen Mayaya ameeleza mafanikio waliyoyapata kwa mwaka 2021/2022 katika miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Mabweni na Kumbi za mihadhara kwa kutumia fedha za vyanzo vya ndani ya chuo na Ruzuku kutoka Serikalini na kueleza matarajio yao ya 2022/2023 ya kujenga Maktaba kubwa na ya kisasa pamoja na bweni la wanafunzi katika eneo la Kisesa Jijini Mwanza.
"Matarajio yetu kwa mwaka 2022/2023 ni kuanza ujenzi eneo la Miyuji Bweni na Kantini, aidha tunategemea kuanza ujenzi wa maktaba kubwa ya kisasa kule Mjini Mwanza pamoja na bweni la wanafunzi "
"Ameongeza kuwa,chuo kimetekeleza jumla ya miradi 8 ya ujenzi kwa fedha za ruzuku kutika Serikalini, Mabweni 2 na Kumbi za mihadhara 3 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 9.7. Miradi inayotekelezwa na mapato ya ndani ya chuo ni miradi 3 ikiwemo jengo la Mgahaw, jengi la Utawala na Maktaba kwenye kituo cha mafunzo cha kanda ya Ziwa Mwanza yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.2"
"Katika mafanikio ya 2021/2022 pia tumefanya upanuzi maeneo ya chuo katika kituo cha mafunzo Mwanza ikiwemo kulipa fidia kwa wananchi waliopisha maeneo, hii inaendana na ongezeko la wanafunzi watakaofanya udahili nayo thamani ni Bilioni 1.7 kutoka katika vyanzo vya ndani vya chuo"
Akisoma hotuba kwa niaba ya wanafunzi wenzake muhitimu Gift Kyando wa kozi ya Bachelor Degree In Environmental Planning and Management, kwanza ameishukuru Serikali na Wizara ya Fedha na Mipango ambayo ni Wizara Mama ya chuo chao na kuomba Chuo kuendelea kuwasaidia ili waweze kusonga mbele zaidi hasa wanapohitaji kupata Barua za uthibitisho kutoka Chuoni hapo.
"Kwanza kabisa kwa niaba ya wanafunzi wenzangu tunaohitimu leo tunaishukuru Serikali yetu na Wizara ya fedha ambayo ndio Wizara Mama ya Chuo chetu cha Mipango lakini pia thnaomba Chuo kiendelee kutusaidia katika mambo mbalimbali tutakayohitaji ili kuendelea kusonga mbele hasa pale tutakapohitaji kupata Barua za uthibitisho kutoka chuoni hapa"
Haya ni mahafali ya 36 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini ya mwaka 2022 ambapo wanafunzi 6225 wamehitimu wakiwemo wanaume 2722 na wanawake 3502 katika fani mbalimbali za Maendeleo vijijini.
Comments
Post a Comment